Membe: Tunaiunga mkono Palestina

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema Tanzania itaendelea kuwaunga mkono watu wa Palestina katika jitihada za kutafuta uhuru wa taifa lao kutoka kwenye mgogoro wa kisiasa kati yao na Israel.
Waziri Membe aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mshikamano na wananchi wa Palestina, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

Akitoa hotuba katika maadhimisho hayo, Waziri Membe alisisitiza kile alichokiita msimamo wa siku nyingi wa Tanzania juu ya mgogoro huo wa Mashariki ya Kati, ambao ni kutaka kuwapo kwa mataifa mawili huru likiwamo la Palestina huru itakayoishi katika mazingira ya amani na usalama na Israel.

“Tutaendelea kuusimamia msimamo wetu wa tangu mwaka 1961 na kushirikiana na watu wa Palestina katika jitihada za kutafuta uhuru wao kwa njia ya amani,” alisema Waziri Membe.

Mara kwa mara serikali imekuwa ikiurejea msimamo huo wa kidiplomasia inapotoa rai yake kwa jumuiya za kimataifa likiwemo taifa la Marekani katika kumaliza uhasama wa mataifa hayo mawili.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita serikali kupitia kwa balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue, ilipongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya Marekani za kuanzisha tena mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina.

“Tanzania pia inaunga mkono suala la kuwapo kwa mataifa mawili huru likiwamo la Palestine huru wakiishi sambamba katika mazingira ya amani na salama na taifa la Israel huku tukiunga mkono haki ya Waisrael kuishi kwa amani,” alisema Balozi Sefue mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipokuwa likijadili taarifa ya Kamati Maalum iliyohusika na uchunguzaji wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi wa Palestina unaofanywa na Israel, mwanzoni mwa mwezi Novemba, mwaka huu.

Kwa upande wake, Balozi wa Palestina nchini, Dk. Nasri Khalil Abu Jaish, aliishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono na kuisaidia Palestina katika jitihada za kuufikia uhuru kamili wa taifa hilo.

Aidha, balozi Abu Jaish alizitaka Jumuiya za Kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa kuingilia kati mgogoro wa Mashariki ya Kati na kuhakikisha watu wa Palestina wanapewa ardhi na uhuru wao unaodhibitiwa na Israel.

0 comments: