Duru za siasa kutoka ndani ya chama hicho tawala zinasema kuwa wakati familia ya Malecela aliyepata kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, ikiumizwa kwa Anne Kilango Malecela kuachwa kwenye baraza hilo, familia ya Makamba nayo imepata maumivu hayo baada ya mtoto wao, Januari Makamba aliyetazamiwa kupewa uwaziri, kuachwa nje.
Vyanzo vyetu vya habari vililiambia Tanzania Daima Jumatano kuwa Januari Makamba tangu alipotangaza nia ya kuwania jimbo la Bumbuli na kupita bila kupingwa, amekuwa akitajwa na watu wengi nje na ndani ya CCM kwamba angeweza kuteuliwa kuwa Waziri au Naibu wa wizara yoyote.
Sababu zilizokuwa zikimpa Januari nafasi ya kuteuliwa kushika uwaziri ni pamoja na kudaiwa kuwa kijana mwenye elimu nzuri huku sifa hiyo ikiwa imetamkwa mara kadhaa na Rais Kikwete mwenyewe.
Sanjari na kuwahi kummwagia sifa kijana huyo, Rais Kikwete pia kwa upande mwingine aliwahi kuahidi huko nyuma kwamba baraza lake lijalo lingekuwa la vijana zaidi.
Sababu nyingine ni Januari kuwa karibu na Rais Kikwete akifanya naye kazi Ikulu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kama msaidizi wake wa karibu, huku uswahiba wa baba yake, Mzee Makamba, na mkuu huyo wa nchi pia ukipewa nafasi.
“Januari mwenyewe alijua angeteuliwa, Mzee Makamba alijiridhisha kabisa kwamba mwanaye angekuwemo kwenye Baraza, lakini uteuzi uliofanywa na Rais umemuumiza sana Mzee Makamba na hadi sasa haamini kilichotokea,” alisema mmoja wa wana CCM kutoka ofisi ndogo ya Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, wadau wa siasa kutoka ndani na nje ya CCM bado wanampa nafasi kubwa Januari kuteuliwa kwenye moja ya wizara zisizo na manaibu kwa sasa au wakati wowote Rais atakapoamua kufanya mabadiliko madogo au makubwa.
Wakati familia ya Makamba ikiuguza maumivu hayo, familia nyingine ya mkongwe wa siasa nchini, Malecela, nayo imeachwa na maumivu kutokana na Anne Kilango pia kuachwa nje ya uteuzi.
Mama Kilango, mmoja wa wanasiasa waliojipatia sifa katika Bunge la tisa lililopita kutokana na ujasiri wake wa kuwalipua mafisadi hadi kutunukiwa Tuzo ya Martin Luther King, amekuwa akitajwa na duru za siasa kwamba angekuwemo ndani ya baraza jipya.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinadai kuwa katika uchaguzi wa mwaka huu, Mama Kilango alipata kuahidiwa kuwa Waziri, lakini aliambiwa aongeze elimu na mwaka jana alitunukiwa shahada yake ya kwanza ili kujiweka sawa kwa uongozi huo.
“Mama Kilango amesoma, amepata digrii yake ya kwanza, anajiandaa kuingia tena darasani apate digrii ya pili na hii yote ni kutokana na kuahidiwa uwaziri, lakini alipewa sharti aongeze elimu,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Sababu nyingine inayotajwa kumpa maumivu Malecela ni ukweli kwamba yuko nje ya Bunge na hana nafasi yoyote muhimu kwenye chama, ukiachilia ile ya kuwa mjumbe wa kudumu wa Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu wa CCM.
“Malecela kwa sasa si Mbunge na alipoangushwa kwenye kura za maoni, alilalamika ndani ya chama akitarajia huruma ya Rais, lakini aliachwa, hivyo uteuzi wa Mama Kilango kuwa Waziri, ungempa faraja kubwa,” alisema mtoa habari wetu.
0 comments:
Post a Comment