Suala la viti maalum lilikuwa na utata mkubwa ndani ya Chadema kabla ya uchaguzi mkuu na kusababisha viongozi watofautiane, lakini mwishoni uongozi wa juu walikubaliana kumtafuta mtaalamu ambaye alitengeneza vigezo na sifa ambazo zilitumika kupata wabunge wa viti maalum, kikiwemo kigezo muhimu cha elimu, uzoefu na kuthubutu kugombea ubunge majimboni. Kwa mujibu wa mchanganuo huo wa kupata wabunge wa viti maalum, Musori alikuwa amepata alama za chini ambazo zingeweza kumpa ubunge tu iwapo Chadema ingefanya vizuri zaidi kwenye uchaguzi mkuu.
Lakini idadi ya kura za urais ya asilimia 26.2 na idadi ya wabunge 24 walioingia bungeni imemfanya mwenyekiti huyo wa wanawake kushindwa kupata nafasi. Lakini Dk Slaa alijibu tuhuma hizo jana akisema kuwa Musori ameondoka kwenye chama hicho baada ya kukosa nafasi ya ubunge wa viti maalum. Alisema mara nyingi watu wanakwenda kwenye vyama wakiwa na maslahi yao binafsi, wasipopata kile walichofuata huanza kunyea kambi, jambo ambalo Dk Slaa alisema linawafanya wazunguke kila chama kwa ajili ya kutetea maslahi yao binafsi. “Ninamshangaa sana Mama Musoril; baada ya kushindwa kupitishwa kwenye nafasi ya viti maalum ameanza kunyea kambi. Mwache aondoke; narudia tena, kama kuna mtu mwingine naye amefuata uongozi ndani ya chama aondoke.
Hakuna huruma katika hilo,” alisema Dk Slaa. Aliongeza kuwa mchakato wa kutafuta wagombea wa viti maalum ulianzia ngazi ya wilaya ambako mama huyo alishindwa kwa kupata kura moja. Baada ya kuona hivyo akaamua kuomba msaada, lakini walishindwa kutokana na majina hayo kufikishwa Tume ya Uchaguzi (Nec) kwa ajili ya kuyathibitisha. Alidai kuwa kutokana na hali hiyo mama huyo alikosa nafasi na ndio maana ameamua kuhama chama. Alisema jambo hilo linaonyesha wazi kuwa alifuata ubunge ndani ya Chadema.
Alikanusha madai ya ukabila akisema kilichopo ni maadili ndani ya chama na kwamba ikiwa mtu ameshindwa, anapaswa kuondoka na kujiunga na vyama vingine. “Kwanza mimi hata dini yake siijui... tatizo lililopo ni kwamba hakuteuliwa kwenye ubunge wa viti maalum ndio maana amehama,” alidai Dk Slaa. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Musori alisema kuwa kutokana na maamuzi ya wabunge wa viti maalum kufanywa na wanaume bila ya kulishirikisha Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), ameamua kujiengua chama hicho. “Chadema inaongozwa kwa misingi ya udhalilishaji wa kijinsia, ukabila, undugu na mambo mengine ambayo si mazuri," alidai Musori. "Jambo hilo limesababisha viongozi wakuu kuchagua majina mengi ya wabunge wa viti maalum ambao hawana uwezo,” alisema Musori.
Alidai kuwa mwenyekiti wa Chadema ndio mwenye maamuzi ya mwisho ndani ya chama na anafanya hivyo bila ya kushirikisha wanachama wake katika kutoa maamuzi hayo, jambo ambalo alidai linasababisha kuwepo kwa mpasuko ndani ya chama. Alisema kutokana na hali hiyo, Chadema inakabiliwa na mpasuko mkubwa ambao utasababisha wanachama wengine kuhama kutokana na maamuzi aliyoyaita ya kiubabe yanayofanywa na viongozi hao katika shughuli za chama bila ya kujali utu wa mtu, wala nafasi yake na hivyo kusababisha kuibuka kwa mgogoro. “Mgogoro uliopo ndani ya chama ni mkubwa.
Mpaka sasa umesababisha wanachama wengine kuhama, hii inatokana na maamuzi ya kiubabe yanayofanywa na Mbowe bila ya kuangalia utu wa mtu, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa udhalilishaji wa kijinsia... tumesikitishwa sana,” alisema Musori Alidai kuwa kuondoka kwake ni mwanzo, lakini kuna wanachama wengi ambao mpaka sasa wameanza kurudisha kadi huku wengine wakiendelea kutafakari uamuzi wa kukihama chama hicho. “Iweje mwenyekiti awe signatory (mtia saini) wa kila kitu, hapo kuna tatizo... haiwezekani kiongozi kuwa na maamuzi yako huku wanachama wanataka vile... kutokana na hali hiyo nataka kujenga heshima yangu na familia; nimeamua kuihama Chadema na kujiuzulu uongozi wowote ndani ya chama hicho na sasa najiunga na NCCR,” alisema. Musori alikuwa mwenyekiti wa umoja huo wa wanawake wa Chadema, mjumbe wa kamati Kuu, mjumbe wa Bawacha na Mweka hazina wa Umoja wa Madiwani wa Chadema).
Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi, James Mbatia alisema suala la maamuzi ndani ya chama linapaswa kufanya na viongozi wa aina zote bila ya kujali jinsia ya mtu au cheo chake na kwamba jambo hilo linaweza kusaidia chama kusonga mbele. “Tunachpaswa kufanya ni kuthamini utu wa mtu,” alisema Mbatia ambaye aligombea ubunge wa Jimbo la Kawe bila ya mafanikio. Huwezi kudai mabadiliko ya katiba wakati katiba ya chama chako inakusuta, kutokana na hali hiyo viongozi wa vyama wanapaswa kujiangalia kwanza kabla ya kutetea kile wanachokitaka. Uamuzi wa Musori umefanyika siku moja baada ya mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Mbeya, Smabwe Shitambala kutangaza kujivua wadhifa wake ili kupisha uchunguzi dhidi yake kufanyika kwa uhuru.
Shitambala, ambaye aligombea ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini na kushindwa na mgombea wa CCM, anadaiwa kupewa fedha na maofisa wa chama hicho tawala ili akihujumu. Shitambala aliwahi kugombea ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mdogo uliofanyika mwaka 2008, lakini alienguliwa na Tume ya Uchaguzi baada ya kubaini kasoro kwenye hati yake ya kiapo. Chadema, ambayo imeibukia kuwa chama kikuuu cha upinzani Tanzania Bara, pia kilipoteza wanachama wake kabla ya uchaguzi mkuu baada ya David Kafulila kukihama mapema mwaka huu na kujiunga na NCCR Mageuzi ambayo ilimsimamisha kuwania ubunge wa Kigoma Kusini na kushinda. Pia ilimpoteza Felix Mkosamali (Muhambwe) na Moses Machali (Kasulu Mjini).
0 comments:
Post a Comment