Vikumbo umeya kila mahali

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KINYANG'ANYIRO cha kutafuta wagombea wa nafasi za umeya katika manispaa mbalimbali nchini umezidi kupamba moto huku madiwani 40 wakijitokeza kuwania nafasi hiyo jijini Dar es Salaam na wengine wakilazimika kujing'atua kutokana na kuwa na elimu ndogo.
Vita hiyo ya umeya ni kubwa jijini Dar es Salaam ambako manispaa za Temeke na Kinondoni zinatafuta mabosi wapya baada ya waliokuwa wakishikilia nafasi hizo kubwagwa katika mchakato wa uchaguzi na wengine kuamua kutowania tena.

Katika Manispaa ya Kinondoni ambapo nafasi hiyo ilishikiliwa na Shaban Londa, hadi jana madiwani 15 kutoka vyama vya CCM na Chadema walikuwa wamejitokeza kuwania umeya, huku nafasi ya naibu meya ikiwawaniwa na wagombea nane.
Idadi hiyo inafanya kuwepo na jumla ya wagombea 22 wa nafasi hizo kutokana na mmoja wa wagombea kutoka CCM kuwania nafasi zote mbili iumeya na unaibu.

Manispaa ya Temeke ambako kiti hicho kiliachwa wazi na Jerome Bwanausi ambaye kwa sasa ni mbunge wa Lulindi (CCM), jumla ya madiwani 13 wamejitokeza kuwaniakiti hicho, wawili kati yao wakiwa wamejitosa kuusaka unaibu na moja unaibu meya wa Halimashauri.

Jana katibu wa CCM wa Wilaya ya Temeke, Saada Kusilawe aliimbia Mwananchi kuwa hadi kufikia saa 10:00 leo jioni, wahusika wanatakiwa kukamilisha taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kurudisha fomu tayari kwa kujadiliwa.
Kusilawe alitaja majina kumi ya wagombea wa nafasi ya meya katika Manispaa ya Temeke kuwa ni Cecilia Macha kutoka Kata ya Mianzini), Kapteni Kenny Makinda (Yombo Vituka), Ali Shaban (Mtoni), Noel Kipangule (Chang’ombe) Francis Mtawa (Keko), Zena Mgaya (Tandika) Anderson Charle (Kijichi), Victor Mwakasendile (Makangalawe) na diwani wa Kata ya (Pemba Mnazi) ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja.

Katibu huyoaliwataja madiwani wanaowania unaibu meya kuwa ni Abdallah Chaurembo (Charambe), Mhidini Fanya (Kimbiji) na Wilfred Kimati (Kurasini) ambaye pia anawania nafasi ya unaibu wa Halmashauri ya Jiji.

Naye katibu msaidizi wa CCM wilayani Kinondoni, Abihudi Shilla alitaja majina ya madiwani watano waliojitokeza kuwania nafasi ya umeya na unaibu wa Manispaa ya Kinondoni kuwa ni Ibrahim Kisoky (Goba) Richard Chengula (Kigogo) na Tarimba Abass (Hananasif).
Madiwani wawili waliojitosa kuwania nafasi ya naibu meya ni Mohamed Chambuso (Mzimuni) na Bernadeta Rich (viti maalumu), alisema.

Ongezeko hilo linafanya madiwani wanaowania nafasi hiyo kufikia 20 na CCM pekee ina wagombea 15 na Chadema watano.
Katika hatua nyingine, mchakato huo kwa Manispaa ya Ilala uliendelea kwa kazi ya kurudisha fomu kwa wanachama watano.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala Ernest Chale aliwataja wagombea wanne ambao tayari wamerudisha fomu hizo hadi jana kuwa ni Abuu Juma mgombea anayetetea kiti chake, aliyekuwa msaidizi wake Jerry Slaa ambao wanatajwa kuwa na mchuano mkali kubwa katika uchaguzi huo, Kisalala Salumu na Dk Didas Masaburi.

Akizungumzia mchakato huo, Chale alisema kazi ya kutoa na kupokea fomu itakamilika leo saa 10:00 jioni na kwamba baada ya muda huo ofisi yake itaanza mchakato wa vikao vya kupitia na kupitisha majina ya wagombea.
Kutoka Mtwara inaripotiwa kuwa madiwani wateule wanne wa CCM wamejitokeza kuwania ya nafasi ya umeya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, huku Meya aliyemaliza muda wake akiamua kutotetea nafasi yake.
Meya huyo, Ali Chinkawene ambaye ni diwani mteule wa Kata ya Majengo, anadaiwa kuhofia ushindani mkubwa unaotokana na wapinzani wake kuwa na elimu kubwa.

Akizungumza na gazeti hili, Chinkawene alisema uamuzi wa kutowania tena nafasi hiyo hauna shinikizo kutoka kwa mtu yeyote na kwamba ameamua kwa hiyari yake.
Kuhusu elimu yake alisema: “Kwa elimu yangu hiyo ya msingi nimekuwa meya kwa miaka mitano. Watu wanapima nimefanya nini katika kipindi hicho kwa kuwa elimu pekee bila ufanisi kwenye kazi haina maana…suala la elimu halina msingi wowote,” alisema.

Katibu wa CCM wa Mtwara-Mikindani, Masoud Chitende aliwataja waliorejesha fomu kuwa ni Salma Chiputa, Seleman Mtalika (Shilingi), Abdallah Starehe na Fatuma Namtumba.
Wilayani Masasi na mji wa Masasi madiwani 12 wamejitokeza kuwania uwenyekiti wa halmashauri hizo.
Katibu msaidizi wa CCM wa wilaya ya Masasi, Shaibu Ngatiche alisema katika Halmashauri ya Masasi, Edward Mmavele aliyewahi kuwa mwenyekiti mwaka 2000 hadi 2005, Jafari Mkwanda na Satima Mohamedi wamerejesha fomu za kuwania umeya.

Wengine ni Adrian Kamteule, Anthony Chihako na Juma Mwaya, wakati kwa upande wa halmashauri ya mji wanaowania ni Andrew Mtumusha, Philimon Millanzi, Alberth Mlambala, Blandina Nakajumo, Mahafudhi Saidi na Ausi Mnela.
Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu, madiwani wateule wawili wamejitokeza kuwania uenyekiti ambao ni Dua William Nkuruwa anayetetea kiti chake na Rajab Athuman Mrope wa Kata ya Mikangaula.
Katika mkoa wa Ruvuma, joto la uchaguzi wa umeya pia limepamba moto baada ya madiwani wengi kujitokeza.
Waliojitokeza kwenye Halmashauri ya Namtumbo ni mwenyekiti wa zamani, Steven Nana, Daniel Nyambo, Gideon Mpilime, Grace Kapinga, Vitus Ngonyani na Alifa Majumba huku nafasi ya umakamu mwenyekiti ikigombewa na Alpius Mchucha pamoja na Cassim Ntara.
Katika Halmashauri ya Songea Vijijini wagombea wawili wamejitokeza ambao ni mwenyekiti wa zamani, Jumanne Nyingo na Rajab Mtiula wakati nafasi ya umakamu inawaniwa na Andrew Mhagama pekee. Kwenye Manispaa ya Songea wamejitokeza wagombea wanne ambao ni Gerlald Ndimbo, Ally Manya, Christon Matembo pamoja na Sharif Mgwasa huku nafasi ya naibu meya hadi ikiwaniwa na Mariam Dizumba.

Mwanza mpambano mkali

Habari kutoka mkoani Mwanza zinasema kuwa mchakato wa kuwania kiti cha umeya wa Jiji umeanza huku Chadema ikipewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea kutokana na wingi wao, hali inayoelezwa kuwa imesababisha zoezi la kuchukua fomu kwa CCM kudorora.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Nyamagana, Mussa Matoroka aliiambia Mwananchi jana kuwa diwani mmoja tu aliyemtaja kwa jina la Stanslaus Mabulla wa Kata ya Mkolani ndiye aliyechukua fomu.
Kwenye jimbo hilo Chadema na CCM zina wagombea watano wa umeya kila chama, wakati kwa Jimbo la Ilemela Chadema ina viti sita wakati CCM ina viti vitatu tu huku wale wa viti maalum wakiwa bado hawajatangazwa na Tume ya Uchaguzi (Nec).

Katibu wa Chadema mkoani Mwanza, Willson Mshumbusi alisema mpaka sasa chama chake hakijatangaza utaratibu wa uchukuaji fomu kikingojea kukamilika kwa taratibu za chama toka makao makuu na kusema kuwa hawana hofu na kiti hicho na kusisitiza kuwa wamejipanga kukitwaa.
Katika Halmashauri ya Geita, mchuano wa kuwania nafasi ya mwenyekiti umeanza kushika kasi ndani ya CCM, huku wagombea wakipita kujinadi kwa madiwani wenzao kwa staili mbalimbali.
Mpaka sasa mchuano huo umetajwa kuwa mkali zaidi kutokana na kiti hicho kuongozwa na makundi ya ubunge na Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM).

Makundi hayo yanaundwa na watu waliokuwa wanamuunga mkono aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Geita, Ernest Mabina na jingine linalomuunga mkono mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Jeremiah Ikangala.
Kundi hilo linadaiwa kuungwa mkono na baadhi ya viongozi katika halmashauri hiyo, huku kundi jingine likitajwa kuwa ni la mgombea Leonard Bugomola ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU) ambaye anaungwa mkono na kundi kubwa la vijana.
Kaimu katibu wa CCM wilayani Geita, Simon Yaowo alisema wagombea waliokuchukua fomu za kuwania kiti hicho ni Jeremiah Ikangala, Leonard Bugomola, Bichuma Christopher, Joseph Lwiza pamoja na Zainab Mahenge.
Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo wagombea waliochukua ni Ahmed Mbaraka, Edward Semanduto, Elias Chesama na aliyekuwa akishikilia cheo hicho kipindi kilichopita, Christopher Kadeo.

Sura mpya zajitokeza Iringa

Mkoani Iringa sura mpya zimejitokeza kuchukua fomu za kuwania umeya CCM, lakini ukabila unaelezwaq kutawala kampeni za awali.
Katibu wa CCM wilayani Iringa, Charles Charles aliwataja madiwani waliojitokeza kuwania umeya kuwa ni Amani Mwamwindi ambaye anamaliza muda wake, Vitus Mushi kutoka Kata ya Mtwivila.
Wengine ni Mussa Wanguvu (Kihesa), Alphonce Mlagala (Ruaha) na diwani wa Kata ya Mshindo, Daudi Albert.
Kwenye Wilaya ya Bunda mkoani Mara madiwani sita wa CCM wamechukua fomu kuwania uenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Katibu wa CCM wa wilaya, Charles Mwangwale aliwataja waliochukua fomu kuwa ni diwani wa Kata ya Mcharo, Julius Maligeri; Sospeter Munubi (Bunda Stoo), Mwita Mang’era (Guta ), Manase Okore (Namhura ) Sumera Kiharata (Hunyari), pamoja na mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Joseph Marimbe (Sazira).
Mwangwale aliwataja wanachama wanaowania umakamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuwa ni diwani wa Kata ya Nansimo, Sabato Mafwimbo na Sospeter Masambu (Nerumo).

Hata hivyo, Chadema na TLP havijaanza mchakato wa kupata wagombea wake.
Upinzani ndani ya chombo hicho unao madiwani watano wa kuchaguliwa, Chadema ikiwa na wanne na TLP mmoja lakini bado hawajatangaziwa viti maalum.

Chadema yateua mmoja Moshi

Mkoani Kilimanjaro, Chadema imemteua diwani wa Kata ya Bomambuzi, Jaffar Michael kuwa mgombea pekee wa nafasi ya meya wa Manispaa ya Moshi.
Katibu wa Chadema wa Moshi, Adam Mtwange alisema kamati ya utendaji ya chama hicho iliyokutana juzi katika kikao kilichohudhuriwa na madiwani iliafiki uteuzi huo.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu, Chadema ilinyakua viti 17 vya udiwani huku CCM ikiambulia viti vitatu tu.
Kwa mujibu wa Mtwange, kamati hiyo ya utendaji imemteua diwani wa Kata ya Kiborloni, Vicent Rimoi kuwania nafasi ya naibu meya kwa tiketi ya Chadema. Rimoi na Michael walikuwa pia ni madiwani katika baraza lililopita.
Kwa upande wa Moshi Vijijini, vyama vya TLP na Chadema vinapitia vipengele vya mkataba wa makubaliano ambayo yatavifanya kuungana na kuweza kuwa na sauti katika baraza la madiwani.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31, kambi ya upinzani ilifanikiwa kupata madiwani 16 ukilinganisha na 15 wa CCM.
Katika baraza la madiwani linaloundwa na majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini, TLP ina madiwani sabahuku Chadema ikipata nao tisa na CCM 15.

Katibu wa Chadema Moshi Vijijini, Akwiline Chuwa aliliambia gazeti hili jana kuwa katika mkataba wa awali walikubaliana mwenyekiti wa halmashauri atoke Chadema na makamu wake atoke TLP.
Mkoani Mbeya taarifa zinasema kuwa kikao cha kamati ya siasa ya wilaya ya CCM ya Mbeya Mjini kimependekeza majina matatu ya madiwani waliochukua fomu ya kugombea nafasi ya umeya.

Majina yaliyopitishwa na kikao hicho ni Atanas Kapunga ambaye ni diwani wa Kata ya Itiji, Dormuhamed Issa (Isanga) na Juma Simbeyanje kutoka Kata ya Nsowo.

Kutoka mkoani Tanga, CCM leo itategua kitendawili cha nani waliopita katika mchujo wa chama hicho wa kuwania uenyekiti wa halmashauri za wilaya, mji na Meya wa Jiji la Tanga baada ya kamati ya siasa ya mkoa kutoa baraka zake.
Kwa mujibu wa habari ambazo Mwananchi imezipata tayari makatibu wa CCM kutoka wilaya zote nane wamewasilisha mkoani majina ya waliochujwa kutoka halmashauri tisa.

Imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Dar, Abdallah Bakari, Mtwara, Christopher Maregesi,Bunda, Tumaini Msowoya, Iringa, Frederick Katulanda, Mwanza, Joyce Joliga, Songea, Brandy Nelson, Mbeya, Burhani Yakub,Tanga na Daniel Mjema, Moshi

0 comments: