Mawaziri wapania kufanya kweli

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter BAADHI ya mawaziri wateule wameeleza namna watakavyojipanga kukabiliana na changamoto katika wizara zao, na wameahidi kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania na taifa kwa jumla.

Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri wa Nchi mteule Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Mkuchika, alisema wizara aliyopewa ni nyeti na inagusa takribani kila sekta, hivyo atahakikisha anatumia uzoefu na uwezo wake wote kutumikia Watanzania.

Alisema, si mara yake ya kwanza kufanya kazi katika wizara hiyo, aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya kwa miaka 13, na Mkuu wa Mkoa kwa miaka minane.

Wakuu wa mikoa na Wilaya hufanya kazi chini ya Tamisemi, hivyo anatambua changamoto nyingi zinazoikabili wizara hiyo.

“Kwa kweli namshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa imani yake kubwa kwangu, na nina faraja angalau katika wizara hii kutokana na uzoefu wangu, najua nini natakiwa kufanya,” alisema Mbunge huyo wa Newala.

Alisema, wizara hiyo ina jukumu kubwa la kukidhi maisha ya Watanzania na kwamba Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imegusia suala zima la maisha bora kwa Mtanzania na kutokana na uzoefu wake, anaamini ataitekeleza ipasavyo ilani hiyo.

Mkuchika alisema, changamoto mojawapo katika wizara hiyo, ni suala la fedha nyingi kupelekwa katika halmashauri za wilaya, kwa ajili ya shughuli za maendeleo ambapo kwa upande wake, atakuwa mkali na kuzisimamia ili ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa.

“Nitakuwa mkali kwa watakaobainika kutumia fedha hizo kwa ubadhirifu, lakini pia kwa ambao watazembea kufanya kazi zao,” alisema Mkuchika aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Waziri mteule wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alimshukuru Rais Kikwete kwa kumuamini na kumrudisha tena kwenye wizara hiyo.

Ngeleja amepania kuhakikisha kuwa mgao wa umeme nchini unakwisha.

“Katika wizara hii mimi siingii kujifunza, naingia kufanya kazi hasa kuendeleza yale yaliyokwishaanzishwa na Serikali iliyopita, nitashirikiana na wataalamu wa umeme na kupitia vyanzo vyote vya umeme, kama vile maji, gesi na mafuta kuhakikisha Tanzania haikumbwi tena na tatizo la umeme,” alisema Ngeleja.

Alisema, iwapo katika uongozi wake tatizo hilo litatokea, litakuwa limetokana na sababu zisizozuilika, kama vile hitilafu katika mitambo tena yote kwa pamoja, jambo ambalo atahakikisha wataalamu wanalishughulikia ipasavyo ili lisitokee.

Aidha, alisema atahakikisha anasimamia mipango ya miradi ya umeme ambayo kwa sasa iko katika hatua za utekelezaji na kuitaja miradi hiyo kuwa ni mradi kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), unaotekelezwa katika mikoa 16.

Kwa mujibu wa Ngeleja, mradi huo unagharimu zaidi ya Sh bilioni 103. Mwingine ni mradi ulio chini ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ambao uko katika mikoa sita na mradi unaofadhiliwa na Benki za Maendeleo ya Afrika (ADB) na Benki ya Dunia ambao uko katika mikoa zaidi ya 10.

Kuhusu sekta ya madini, Ngeleja alisema ana mpango wa kuhakikisha utafutaji wa mafuta na gesi unaboreshwa na kuzingatiwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mpango wa kuingiza mafuta nchini kwa pamoja unatekelezwa kwa haraka ili kupunguza msongamano wa meli bandarini.

Alisema, atahakikisha utekelezaji unazingatia zaidi sera ya madini ya mwaka 2009 na Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010 ambazo zote zimelenga kuboresha zaidi manufaa kwa Taifa na wananchi katika sekta hiyo ya madini.

Waziri wa Nchi mteule Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira, alisema Wizara yake imegawanyika katika sehemu mbili, ikiwamo inayogusa jamii na inayoratibu mipango ya maendeleo kama vile Mkurabita na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF.

Alisema kwa upande wa uratibu, akiwa waziri, kwa kushirikiana na wafanyakazi wenzake, watapanga kusimamia na kutathmini utekelezaji wa mipango hiyo ya maendeleo.

Akizungumzia suala la uhusiano, alisema linagusa jamii ambayo imegawanyika katika makundi mbalimbali yakiwamo ya kidini na kisiasa.

“Hapa tutakalojaribu kufanya ni kuhakikisha imani zetu kwa upande wa dini na kisiasa haziondoi msingi wa umoja wetu,” alisema Waziri huyo aliyekuwa katika Baraza lililopita akiongoza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, na pia aliwahi kuongoza Tamisemi.

Alisema kila Mtanzania kwa mujibu wa Katiba, ana uhuru wa kuamini dini yoyote na chama chochote kile, ambapo wizara hiyo itahakikisha uhuru huo unabaki ulivyo isipokuwa tofauti za kiimani hazitaingilia umoja na iwapo kutakuwa na tofauti zenye kuhatarisha amani, zitashughulikiwa kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Waziri wa Nchi mteule, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, Samia Suluhu Hassan, alisema anaamini kila waziri aliyechaguliwa na Rais Kikwete, amechaguliwa kutokana na uwezo alionao katika eneo husika.

Samia alisema wizara aliyopewa ana uzoefu nayo, kwa kuwa alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya kutatua kero za Muungano, hivyo anazitambua changamoto za Muungano na jambo atakalohakikisha ni kufanya kazi kwa misingi iliyopo ya Muungano kupitia Katiba mbili ya Zanzibar na ya Muungano.

“Wizara hii ina changamoto kubwa, nitasimama kwenye misingi ya Muungano na kuhakikisha kuwa kero na uamuzi unaotolewa kuhusu Muungano unakidhi pande zote mbili,” alisema Suluhu aliyekuwa Waziri wa Biashara, Utalii na Uwekezaji katika Serikali ya Awamu ya Sita ya Zanzibar ya Rais Amani Abeid Karume.

Waziri wa Nchi mteule, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, aliyerejeshwa katika ofisi hiyo, alisema changamoto kubwa atakayoanza nayo ni kuondoa kero za watumishi, ikiwamo ya upandishaji vyeo.

“Nitaendeleza pale nilipoishia, lakini kubwa ni kuondoa kero zinazowakabili wananchi kama upandishaji wa vyeo na kuhakikisha mishahara inafika kwa wakati, ingawa kwa kiasi kikubwa sasa tatizo hilo limetatuliwa,” alisema Ghasia ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini.

Alisema, atahakikisha urasimu unazidi kupungua katika ofisi za utumishi wa umma kwa kuongeza ufuatiliaji, akifafanua kuwa “kama watumishi watatekeleza kazi zao kama mikataba ya huduma kwa mteja inavyotaka, nasi tukahakikisha hilo linafanikiwa, naamini urasimu hautakuwapo.

“Awamu hii tunataka kutilia mkazo huduma kwa njia ya mtandao, kwani si lazima wananchi kuonana na mtumishi uso kwa uso, ila anaweza kuhudumiwa kwa njia ya mtandao,” alisema Ghasia.

Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu, ambaye katika kipindi kilichopita alikuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, alisema ili uchumi ukue kwa kasi ambayo imeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, atahakikisha kunakuwa na uwekezaji wa kasi kwa kushirikisha Watanzania.

0 comments: