Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Dodoma alipokuwa akizindua rasmi chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambapo aliweza kumteua Rais mstaafu wa awamu ya tatu Benjamini William Mkapa kuwa mkuu wa chuo hicho.
Alisema kuwa serikali yake imeamua kufanya hivyo ili kuhakikisha kuwa tatizo la mikopo linalowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu hapa nchini linakwisha ambapo hadi kufikia Januari mwakani kamati hiyo itakuwa tayari imeshaundwa.
“Tumekuwa tukipokea malalamiko mbali m,bali kutoka kwa wanafunzi wa vyuo hapa nchini hivyo basi kwa kuliona hilo serikali yetu imeamua kuunda kamati itakayo shughulikia matatizo hayo kwa ukaribu kabisa,”alisema Rais Kikwete
Kikwete alisema serikali yake itaendelea kutoa mikopo hata katika vyuo binafsi ili kuwapa nafasi hata wale wasio na uwezo kujiunga na vyuo mbali mbali.
“Wanafunzi wengi wa vyuo vya binafsi wamekuwa wakiilalamikia serikali kutokana na ongezeko la ada katika vyuo hivyo vya binafsi hivyo basi sisi kama serikali tumeamua kuendelea kutoa mikopo katika vyuo hivyo ili kuwawezesha hata wale wasio na uwezo kusoma bila matatizo yeyote
“Sisi kama serikali tunapenda kuwambia kuwa tumesikia kilio chenu na kupitia klamati hii itakayokuwa ikishughulikia masuala ya mikopo na hakika tutafanikiwa kukidhi haja ya kila mwanafunzi bila kujali ni chuo cha serikali ama binafsi,”alisisitiza Dk Kikwete.
Kikwete alimuomba Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mohamed Gharib Bilal kuendelea kufundisha katika chuo hicho somo la Fizikia kutokana na Tanzania kukabiliwa na uhaba wa wataalamu wa fani yake.
“Sitaki watanzania wanilaani kwa kuwaondolea mwalimu wao wa sayansi, Dk Bilal ni Mwalimu katika siasa ameingia tu… Kwanza ukiwa Makamu wa Rais unanafasi kubwa tu, unaweza kuwa na safari ya kikazi ya wiki moja ukaaja hapa ukaendelea kufundisha vipindi vyako vya phisikia,” alisema Rais Kikwete na kufafanua:
“Lakini pia kuna wanafunzi wa PHD (shahada ya uzamivu) uliokuwa unawasimamia, hakuna sababu ya kuwaacha, naomba uendelee kuwasimamia,”.
Wakati Kikwete akiyasema hayo, Dk Bilali ambaye pia alihudhuria sherehe hizo, alionekana mwenye uso angavu uliokuwa na tabasam wakati wote.
Uamuzi huo wa Rais Kikwete kumruhusu makamu wake kuendelea na kazi yake hiyo, unaweka historia ya kipekeke katika historia ya Tanzania kwa kiongozi wa juu siasa kufundisha.
Alitoa mfano kuwa asilimia 76 ya wanafunzi wenye sifa ya kusomea udaktari wamekuwa wakikosa nafasi hiyo kutokana na uhaba wa vyuo vya elimu ya juu vinavyotoa elimu ya tiba na kusababisha Taifa kuwa na idadi ndogo ambayo inakuwa na uwiano wa daktari mmoja kutibu watu 30,000 ambapo lengo la nchi kupata madaktari 1000 kwa mwaka.
Katika hatua nyingine Kikwete amevitaka vyuo vikuu binafsi kulitazama upya suala la ada zinazotozwa na vyuo hivyo na kuacha kupandisha ada hizo ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengi kusoma kutokana na kipato duni walicho nacho.
Alitoa changamoto kwa taasisi binafsi kuendelwea kupanua Vyuo vya elimu ya juu na kuanzisha Vyuo vipya na kwmaba serikali itaendela kutengeneza mazingira bora ili kuwezesha taasisi hizo kuongeza kasi ya kupunguza idadi kubw aya wanafunzi wanaokosa fursa ya kujiunga na elimu ya juu.
“Vyuo vikuu binafsi vitazame upya namna ya kujipanua ili viweze kudahili na kupokea idadi kubwa ya wanafunzi, pia vilitazame upya suala la ada. Visipandishe sana ada maana serikali itashindwa kuwalipia wale wataokuwa wanasoma katika vyuo hivi,”alisema Kikwete.
Kikwete ambaye alidai siri kubwa ya kuwepo kwa nchi tajiri na maskini ni utofauti wa elimu kwa kusema nchi zote zilizoendelea ni zile ambazo zimewekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu hivyo hakuna njia rahisi itayoondoa umasikini hapa nchini zaidi ya kuwekeza katika elimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Rais Mstaafu Benjamini Mkapa aliahidi kuendeleza kasi ya ujenzi wa Chuo hicho hadi kufikia kiwango cha Kimataifa na kufikia lengo la serikali kwa chuo hicho kuwa na idadi ya wanafuzni 40,000 ifikapo mwaka 2015.
Mkapa alisema kuwa kushukuru ni kuomba tena ambapo alizimwagia sifa Taasisi na Mashirika ya Mifuko ya ya Penseni na mifuko ya fedha pamoja na Baraza la Chuo pamoja na wadau mbalimbali wa Elimu ambao ushirikiano wao umewezesha kufikia kwa lengo la Serikali.
Makamu mkuu wa UDOM Prof Idris Kikula alisema Chuo ambacho kilianzishwa miaka mine iliyopita hadi sasa kina wanafunzi 20,000 ambapo leo wanatarajia kuhitimu wanafuzni 1279 katika mahafari ya kwanza ya Chuo ambao watakuwa wakipewa shahada mbalimbali .
0 comments:
Post a Comment