Zitto akalia kuti kavu • DK. SLAA ASHANGAZWA NA TAARIFA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, hivi sasa yuko katika wakati mgumu na huenda akavuliwa wadhifa wa Unaibu Katibu Mkuu.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa kikao cha Kamati Kuu ambayo kilianza jana na kumalizika leo kinaweza kufikia uamuzi huo baada ya wabunge wa chama hicho juzi kuamua kumvua Zitto wadhifa wa Naibu Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Wabunge hao walifikia uamuzi huo baada ya Zitto kutofautiana na msimamo wa chama chake ulioamua kususia hotuba ya Rais Kikwete, Novemba 17 alipokuwa akilihutubia Bunge na kulizindua Bunge hilo la 10.

Zitto, aliamua kuzungumza na vyombo vya habari namna alivyopinga hatua ya chama chake na mchakato mzima ulivyokwenda mpaka wakafikia uamuzi wa kususia hotuba hiyo ambapo wabunge wa chama hicho walitoka katika ukumbi wa Bunge wakati Rais Kikwete alipoanza kuhutubia.

Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu huenda wakapendekeza Zitto, ang’olewe kwenye wadhifa huo huku wakijenga hoja kuwa kiongozi huyo amekosa fursa ya kuaminiwa na wabunge wenzake kuwa Naibu Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni hivyo hana sifa pia ya kuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama.

Hoja inayosimamiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ni kuwa kama Zitto, ataendelea na wadhifa wa Naibu Katibu Mkuu kuna uwezekano wa kuibuka kutokuelewana na wabunge wenzake.

Chanzo hicho kimedokeza kuwa wajumbe hao wanaweza kujenga hoja kuwa kwa kuwa hakuaminika katika nafasi ya Nafasi ya Naibu Msemaji wa Kambi ya Upinzani basi haaminiki hata kuwa Naibu Katibu Mkuu.

“Nina imani kuwa Zitto, anaweza kujiuzulu kwa sababu wenzake wameonyesha kutokuwa na imani naye katika nafasi ya Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, sasa watakuja na hoja ya kutaka aondolewe na kwenye Nafasi ya Naibu Kati Mkuu,” alidokeza mmoja wa wajumbe wa Kamti Kuu.

Juhudi za Tanzania Daima Jumapili, kumpata Zitto kuzungumzia sakata hilo ziligonga mwamba baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.

Zitto, ambaye alilazwa katika Hospitali ya Agha Khan, siku tatu zilizopita akiugua ugonjwa wa homa ya matumbo, anaweza asihudhurie katika kikao cha leo kutokana na matatizo yanayomkabili.

Naye Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, alipoulizwa kuhusu sakata hilo la Zitto, alisema hayuko tayari kulizungumzia kwa kuwa liko juu ya uwezo wake na kikao cha Kamati Kuu ndicho kitakachotoa msimamo wa kiongozi huyo.

Naye Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, alisema suala hilo liko mikononi mwa wajumbe wa Kamati Kuu, hivyo hawezi kuingilia majukumu yasiyo yake.

Dk. Slaa, pia alisema kuwa anashangazwa na taarifa zinazodai kuwa Zitto alikula chakula chenye sumu kwenye mkutano wa wabunge wa CHADEMA uliofanyika Bagamoyo siku tatu zilizopita.

Alisema anayepaswa kueleza ugonjwa wa mtu ni dakatari anayemtibu na si chombo cha habari kilichotoa taarifa kuwa Zitto amelishwa sumu.

Dk. Slaa, alisema tangu kuanza kuugua kwa Zitto, mafisadi na wasioitakia mema CHADEMA wamekuwa na harakati za kueneza propaganda za kutaka kuivuruga lakini kamwe kusudio lao halitofanikiwa.

Alisema juzi akiwa ofisi alitumiwa ujumbe mfupi na Zitto, akimtaarifu kuumwa kichwa na baadaye kukimbizwa hospitali kwa mapumziko na kupatiwa matibabu zaidi.

“Unajua hivi sasa sisi tunajua nini kinachoendelea; maofisa Usalama wa Taifa kwa kushirikiana na mafisadi wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kuisambaratisha CHADEMA kabla ya mwaka 2015, lakini kwa hili sisi tuko makini nalo na agenda ya kuendelea kuwatumikia Watanzania ndiyo tunayoishughulikia sasa na hata kama kuna matatizo huwa tunayamaliza kwa kupitia vikao vyetu kama leo tuko na wajumbe wa Kamati Kuu kwa dharura tukijadili hali ya chama chetu,” alisema Dk. Slaa.

Aliongeza kuwa CHADEMA imekuwa ikiandamwa na mafisadi ambao wengine waliwataja kupitia mikutano ya hadhara katika viwanja vya Temeke, Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam.

Katibu mkuu huyo, alitoa wito kwa Watanzania kupuuza magazeti yanayotoa taarifa za uongo unaoenezwa na mafisadi ili kuwatoa Watanzania katika kujadili maslahi ya taifa lao na umaskini unaowakabili.

Hata hivyo alisema katika kujikinga na maovu hayo watapambana na wale mbao hawaitakii mema CHADEMA na kusisitiza kuwa huu ni wakati wa kazi na kuonyesha vitendo hasa kwa kupambana na uovu mbele ya macho ya Watanzania.

Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kuipaka matope CHADEMA kwa kupakaziwa matope na kuonekana kuwa haifai mbele ya macho ya jamii kwa ujumla.

“Ndugu yangu hata siku moja usitegemee chombo cha habari ambacho mmiliki wake tulimlipua kwa ufisadi halafu wewe akakuandike vizuri; katu haliwezekani nasi tunajua nini huyo fisadi anachokifanya yeye pamoja na timu yake, CHADEMA iko shwari ila wanataka kutumia mbinu zao za kijasusi kuimaliza hapa hawawezi kabisa,” alisema Dk. Slaa.

Katika kikao hicho cha dharura kilichoitishwa chini ya mwenyekiti wake Freeman Mbowe, kinajadili mambo mbalimbali yaliyotokea katika kipindi cha miezi miwili na kupata ufumbuzi wake.

0 comments: