Dk. Slaa aanza mashambulizi • ASEMA MAFISADI WASUBIRI KIAMA CHAO

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIBU mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa, amesema kuwapo kwake nje ya Bunge hakumfanyi aache kupambana na mafisadi na vitendo vya kifisadi.

Dk. Slaa, alisema mafisadi wanaodhani kutokuwapo kwake bungeni ndiyo salama yao wanajidanganya kwani ataendeleza mapambano yake aliyoyaanzisha akiwa bungeni nje ya Bunge.

Aliitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akipokea tuzo ya Majimaji iliyotolewa na kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kutokana na kazi yake aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitano katika Bunge la tisa.

Tuzo hiyo hutolewa na LHRC kama ishara ya kuwakumbuka watu wote waliopigana katika Vita vya Majimaji na hivi sasa wamekuwa wakiitoa kwa watendaji wa mahakama na wabunge wanaofanya vizuri katika shughuli zao za kiutendaji.

Dk. Slaa, alisema wakati akiwa bungeni alikuwa akitimiza wajibu wake wa ibara ya 14 na 15 inayoweka bayana wajibu wa mbunge katika kupiga vita ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma.

Alibainisha kuwa mbunge yeyote ambaye hakemei au kuuchukia ufisadi anakiuka ibara hiyo lakini pia hafai kuwa kiongozi.

Alisema kuwa mafisadi kamwe wasitarajie wamepata ahueni kwa yeye (Slaa) kuwa nje ya Bunge bali hivi sasa ndiyo atazidisha kasi ya mapambano ya ufisadi ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika ipasavyo.

“Mafisadi wajue hivi sasa ndiyo nitakuwa mkali zaidi, wasitarajie kuwa kutokuwapo bungeni kutanifanya nipunguze kasi ya kupambana nao,” alisema.

Alibainisha kuwa amefurahi kupata tuzo hiyo ambayo itachangia wanasiasa wengi kutimiza wajibu wao kwa ukamilifu hasa baada ya kugundua kuna taasisi zinafuatilia kazi wanazozifanya ndani na nje ya Bunge.

Mkurugenzi wa LHRC, Fransis Kiwanga, ambaye alimkabidhi tuzo hiyo Dk. Slaa kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi Askofu mstaafu Elinaza Sondoro, alisema wamempa tuzo hiyo baada ya kufanya uchunguzi wa kina kwa kupitia mitandao mbalimbali na kutoa dodoso katika maeneo ya vijijini ambapo Dk. Slaa alishinda kwa asilimia mia moja.

Kiwanga, alisema mbali na mitandao pia waliwatumia wafanyakazi wa Bunge ambao walipitia majadiliano ya Bunge (hansard) yaliyoonyesha utendaji kazi wa Dk. Slaa.

Alibainisha kuwa walibaini kuwa Dk. Slaa, alifanya kazi zake kwa kuzingatia sheria na haki za binadamu hasa katika uulizaji maswali ulioibua mijadala mbalimbali ukiwemo ule wa EPA na Richmond.

“Dk Slaa alikuwa akilitetea taifa kwa nguvu zake zote hasa katika uulizaji wake maswali ulioibua mijadala mbalimbali kama ule waraka wa EPA alioutoa bungeni wakati wa hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu wa mwaka 2007,” alisema Kiwanga.

Alisema Dk. Slaa wakati akiwa mbunge aliweza kuwasilisha hoja yake binafsi ya kutaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge Agosti 13, 2007 ili kuchunguza matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hoja nyingine binafsi aliyoitoa Dk. Slaa ambayo ilikuwa inazingatia haki za binadamu ni ile iliyohusu mkataba wa kufua umeme wa Kampuni ya Richmond ambapo alitaka kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza mkataba huo.

Kutokana na hoja hiyo, kamati teule iliundwa na ilibainisha kuwapo kwa utata katika mchakato mzima ulioipa ushindi kampuni ya Richmond.

Alisema jambo jingine alilolifanya Dk. Slaa ni kuibua hoja ya mkataba wa serikali kwa kampuni ya Alex Stewarts juu ya kuhakiki mapato yatokanayo na dhahabu.

Aliongeza pia alifanya hivyo pale alipohoji uhalali wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kulipa deni la kampuni ya Meremeta kiasi cha sh bilioni 155 kinyume na taratibu.

Pia alihoji mikataba ya kampuni ya Mwananchi Gold na Deep Green Finance ambapo Benki Kuu ililipa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 5.51 (zaidi ya bilioni 5).

Kuhusu historia ya tuzo ya Majimaji, Kiwanga alisema tuzo hii ni ya pili kutolewa ambapo hutolewa kwa watendaji wa Mahakama na Bunge.

Alisema kuwa tuzo ya kwanza ilitolewa kwa mhimili wa Mahakama ambapo Jaji Mwalusanya alikabidhiwa mwaka 2005.

Naye mjumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kituo hicho, Dk. Sengondo Mvungi, alisema Watanzania wanaonewa sana kwa kubebeshwa na watendaji walio mstari wa mbele kutafuna rasilimali za taifa.

Alisema deni linalodaiwa na Shirika la Umeme (TANESCO) ni lile la kampuni ya Dowans ambayo iliifikisha TANESCO katika mahakama ya kimataifa ya biashara kupinga kukatishwa kwa mkataba wa kuzalisha umeme.

Alibainisha kuwa hakuna Mtanzania atakayesimama na kupinga deni hilo hivyo taifa linahitaji watu aina ya Dk. Slaa kupinga uonevu unaofanywa kwa Watanzania.

Dk. Mvungi alisema deni linalotakiwa kulipwa na TANESCO la sh bilioni 185 ni kubwa sana lakini hakuna Mtanzania atakayekuwa na ujasiri wa kusimama na kuhoji na badala yake watakubali kulipa bila ya kujua deni hilo litalipwa kwa kupitia ankara watakazokuwa wakizipata!

“Hili deni la Dowans, ni lazima litalipwa hatuna ujanja, tunahitaji watu wa kukemea uonevu wa aina hii kama anavyofanya Dk. Slaa,” alisema Dk. Mvungi.

0 comments: