Mwanzoni mwa wiki hii Waziri mpya wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alimtaka Mrema afanye kazi huku akiamini haondoki katika wadhifa huo na aweke matumaini ya kuishi kwa miaka 100.
Kwa kirefu Mrema amekuwa akiandamwa na tuhuma mbalimbali za kifisadi katika wakala huo, ikiwa ni pamoja na kudaiwa kuvunja mikataba na makandarasi bila kufuata taratibu.
Hata hivyo, taarifa za kuaminika ambazo Tanzania Daima inazo kutoka TANROADS, zilieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa jana baada ya viongozi wakuu wa wizara hiyo kukutana na kujadili juu ya suala la Mrema na kufikia hatua ya kumuengua.
“Huu uamuzi umefikiwa leo na viongozi wetu wakuu, kwa kweli tumefurahishwa sana maana ukiangalia kwa kipindi chote alichokaa katika uongozi wake Wakala huu umepoteza sifa, huku akivunja mikataba kila mara ya makandarasi bila kufuata utaratibu,” alisema mtoa taarifa wetu.
Alisema kuwa Mrema hajafurahishwa na uamuzi huo ambapo inadaiwa iwapo serikali itaamua kumchukulia hatua atakuwa tayari kuwataja vigogo wote waliokuwa wakiomba fedha ndani ya wakala huo.
Wakati huo huo, taarifa hizo zilifafanua kuwa kwa sasa ameandika barua akieleza kuwa amepata nafasi ya masomo nchini Uingereza kwa ajili ya shahada ya uzamivu ya ‘Civil Engineering’.
Uamuzi huo wa Mrema kuelekea nje ya nchi umeelezwa kuwa ni wa kutaka kukwepa ushahidi, kwa kile kilichoelezwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kuwa inaweza kumchunguza kwa tuhuma za kuisababishia hasara serikali.
0 comments:
Post a Comment