KUKEMEA UOVU SI UDINI - PENGO

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAKATI serikali ikionyesha hofu ya udini kuingizwa kwenye siasa, Kanisa Katoliki limesema kuwa halitaacha kukemea uovu hata kama uovu na uozo huo unafanywa na watu walio madarakani kwa kuwa kufanya hivyo si udini.

Mara kadhaa wakati wa kampeni na baada ya kuapishwa Rais Kikwete alikuwa akizungumzia hofu yake ya udini kuingizwa kwenye siasa na akaweka bayana suala hilo wakati wa hotuba yake kwenye Bunge jipya, ingawa hakufafanua jinsi udini ulivyopenyezwa.

Lakini jana, askofu mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Polycap Kadinali Pengo alieleza kuwa hata kama walio kwenye mamlaka watawatishia, kanisa halitakuwa tayari kukaa kimya likiona kuna uovu.

Kardinali Pengo alitoa msimamo huo wa kanisa hilo kubwa nchini wakati akitoa mahubiri yaliyorushwa na kituo cha redio ya kanisa hilo cha Tumaini katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la Utoto Mtakatifu kituo cha Hija kilichopo Pugu jijini Dar es Salaam.

Pengo alisema kuwa viongozi wa Kanisa Katoliki hawawezi kufumbia macho uovu kwa kuwa hata viongozi wa kanisa wanapofanya uovu hukemewa bila uoga.

"Kamwe kanisa haliwezi kufumbia macho uovu ili kundi moja liweze kukaa kwenye mamlaka na uovu wao. Hata kama mamlaka hiyo itatoa vitisho kwa viongozi wakuu, Kanisa Katoliki halitakaa kimya," alisema Pengo.

Alisema kuwa kukemea uovu kusionekane kuwa ni udini na ifahamike kuwa Kanisa Katoliki halimsimiki mtu awe rais, diwani au mbunge wa mahali popote, hivyo uovu wowote unaofanywa na mamlaka utaendelea kukemewa bila uoga.

"Katoliki linafahamu madhara yanayoweza kujitokeza katika jamii iwapo kanisa litampendekeza mtu kuwa kiongozi," alisema Pengo.

"Tuliombee taifa letu liepushwe na vitu vinavyotaka kuibuka katika taifa na kamwe kanisa haliwezi kumsimamisha mtu na kusema mumpigie kura," alisema.

Alisema hawawezi kuwanyamazia wanasiasa wakati hata maaskofu pia wanakemeana wanapotenda uovu.
"Uovu lazima ukemewe, si kitu ambacho mtu anafikiri kwamba mtu anaweza kutishia kwamba maaskofu wasikemee uovu," alisema Pengo.

Pengo alisema kuwa kutokana na kumbukumbu ya hapo zamani wakati wafalme walikuwa wakichaguliwa na mapadri na maaskofu, madhara yake yalijitokeza kwa kuwa jamii ilichaguliwa kiongozi asiyekubalika.

"Viongozi wa Katoliki wataendelea kukemea uovu huo kwa kuwa unaweza kusababisha mafarakano katika taifa linalotafuta ukweli na haki kwa ajili ya wote,"alisema Pengo.

Katika taifa lililo na watu takriba milioni 35 linaloundw ana idadi kubwa ya Wakristo na Waislamu wanaoshi pamoja, udini hauonekani kuwa silaha ya ushindi kwenye siasa.

Lakini suala hilo lilizungumzwa sana, hasa na viongozi wa chama tawala katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, lakini hakuna aliyekuwa tayari kumnyooshea kidole mtu aliyekuwa akituhumiwa kutumia silaha hiyo ili ashinde.

0 comments: