Kigogo aiingizia Tanesco hasara ya mamilioni

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Msemaji wa Tanesco, Badra Masoud

UJEURI wa kigogo mmoja ndani ya Shirika la Umeme (Tanesco) wa kutosikiliza mafundi wake, umesababisha transfoma kubwa inayofanya kazi katika njia kubwa ya umeme wa gridi ya taifa, kituo cha Kipawa kuungua, Mwananchi limebaini.
Kuungua kwa transfoma hiyo kumesababisha wakazi wa mkoa wa Dar es Saalam kuingia katika mgawo wa umeme wa lazima wa saa nne hadi sita kila siku na ambao Tanesco imesema utadumu kwa wiki tatu.

Mgawo huo unaelezewa umeisababishia Tanesco hasara inayokadiriwa kufikia Sh 1 bilioni, kutokana na gharama za kuagiza transfoma nyingine pamoja na makusanyo ya fedha ambayo shirika hilo litayakosa kutoka kwa watumiaji umeme viwandani na makazi ya watu kutokana na mgawo huo.

Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya Tanesco zimeeleza kwamba kigogo huyo alitoa amri ya kuruhusu umeme kwa msongo mkubwa kuzidi uwezo wa transfoma hiyo, licha ya tahadhari iliyotolewa na mafundi.
Msemaji wa Tanesco, Badra Masoud alithibitisha kuharibika kwa transfoma hiyo yenye uwezo wa kudhibiti umeme wa msongo wa megavolti Ampaya (MVA) 45.

Ingawa msemaji huyo alisisitiza kwamba kuharibika kwa transfoma hiyo ni hitilafu ya kawaida, habari za kuaminika zimeeleza kuwa ni uzembe wa kigogo huyo mwenye taaluma ya uhandisi wa umeme.
Kulingana na habari hizo za ndani ya Tanesco, kigogo huyo ambaye jina tunalihifadhi, wiki iliyopita alitoa amri kwamba mafundi warekebishe transfoma hiyo ifanye kazi kwa kiwango cha juu ili kuondoa matatizo ya umeme yaliyokuwepo katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam.

“Aliambiwa na mafundi wake kwamba kufanya hivyo ni hatari kwa sababu transfoma hiyo ni chakavu na baadhi ya vifaa vya kinga dhidi ya hitilafu vimeondolewa,” kilieleza chanzo hicho.
“Lakini … (kigogo) huyo alishikilia msimamo kwamba watekeleze amri hiyo. Mafundi walifanya marekebisho hayo Ijumaa (wiki iliyopita) na siku iliyofuata, yaani  Jumamosi transfoma hiyo ikalipuka na kuungua.”
Chanzo hicho kilieleza kwamba kulipuka kwa transfoma hiyo kulitokana na umeme uliopo katika gridi ya taifa kuwa na kawaida ya kuongezeka na kupungua.

“Unajua umeme wetu haueleweki. Una tabia ya kuongezeka na kupungua. Sasa hali hiyo ilisababisha transfoma hiyo kuzidiwa nguvu na kuungua,” kilieleza chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema: “Unajua bosi huyu ni mtu asiyeshaurika. Ni jeuri; ana taaluma ya uinjinia wa umeme, lakini mafundi wanaofanya kazi na transfoma hizo ndio wanaozijua kuliko yeye.”
Chanzo hicho kilieleza kwamba transfoma hiyo ni chakavu, lakini pia baadhi ya vifaa vya kuilinda na hitilafu ya umeme vimeondolewa.

Kilieleza kwamba vifaa hivyo viliondolewa na baadhi ya mafundi kutokana na amri ya vigogo wa kigeni waliokuwa wanasimamia Tanesco miaka ya nyuma.
“Kuanzia hapo transfoma hiyo, imekuwa ikifanya kazi kwa kiwango cha chini kwa sababu ya mapungufu hayo ya vifaa hivyo vya protection (kuilinda na hitilafu),” kilisema chanzo hicho.
Baada ya tukio hilo, chanzo hicho kilieleza kwamba kigogo huyo alikataa kwenda kutembelea kituo cha Kipawa licha ya wenzake kwenda na kushauriana na mafundi.

Mwananchi lilipowasiliana na Badra, alimtetea kigogo huyo akisema kwamba hahusiki na kwamba hitilafu hiyo ni ya kawaida.

“Transfoma kama hiyo iliwahi kuungua Mbeya. Kwani nani alihusika… Hii ni hitilafu ya kawaida tu, hakuna mkono wa mtu. Huo ni uzushi,” alieleza Badra.
Badra alisema kwa sasa Tanesco ipo katika mkakati wa kuweka Transfoma nyingine ili kuepuka hasara inayoendelea kulikumba shirika hilo.
Msemaji huyo alishindwa kueleza mara moja hasara itakayopatikana wala gharama ya transfoma hiyo ambayo aliilezea ni “kubwa sana isiyoweza kubebwa na magari ya kawaida, ikilinganisha na transfoma nyingine zinazoonekana barabarani.”

Mtaalamu mmoja wa Tanesco alielezea tofauti iliyopo kwamba transfoma za vituo vikuu zina uwezo wa kipimo cha megavolti wakati za kawaida zinazosambaza umeme kwa wateja, zina uwezo unaopimwa kwa kilovolti (KVA).
Hitilafu hiyo, alisema itasababisha mgawo wa umeme kwa maeneo mengi jijini Dar es Salaam kutokana na kituo hicho kuhudumia wilaya zote; Ilala, Temeke na Kinondoni.

Maeneo yatakayoathirika, Badra aliyataja kuwa. ni Segerea, Kinyerezi, Bangulo, Tandika, Temeke, Mtoni, Mashine ya Maji, Yombo Vituka, Yombo Buza, Yombo Kilakala, Mbagala Kilungule, Maeneo ya Viwanda Vingunguti, Karakata, Banana, Kipunguni na Kivule.

Maeneo mengine ni Kitunda, Mwanagati, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Chang’ombe, Temeke, Keko, Mtoni, Barabara ya Nyerere, Barabara ya Kawawa, Tazara, Vingunguti, Kiwalani, Segerea, Bangulo, Yombo Kilakala, Mbagala Kuu, Mbagala Kilungule, Banana, Kivule na Kitunda.

0 comments: