Homa Baraza la Mawaziri yazidi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Rais Jakaya Kikwete ambaye leo anatarajiwa kutangaza baraza la Mawaziiri linalosubiriwa kwa hamu na wananchi nchini Tanzania
Sadick Mtulya 
SHAUKU ya kujua majina ya wanaounda baraza jipya la mawaziri inazidi kuongezeka kiasi cha Ikulu kulazimika kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi, huku kukiwa na taarifa kuwa Rais Jakaya Kikwete anatarajia kulitangaza leo.Tangu Rais Kikwete amteue Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu, kumekuwa na shauku kubwa ya kujua wanaounda baraza hilo na kumekuwa hakuna taarifa ya siku ambayo mkuu huyo wa nchi ataweka bayana majina ya wasaidizi wake.
“Sioni s ababu ya wananchi kuwa na wasiwasi kuhusu Baraza la Mawaziri; kwani kuna jipya hapo,’’ alisema mkurugenzi wa Mawasiliano wa Rais, Salvatory Rweyemamu alipoulizwa siku ya kutangazwa kwa baraza hilo. Badala yake, Salva aliwataka wananchi kutotumia muda mwingi kujadili baraza hilo kwa kuwa si mara ya kwanza kutangazwa.

“Shughuli ya kutangaza Baraza la Mawaziri ni ya rais na atatangaza atakapoamua,’’ alisema mwandishi huyo wa habari wa siku nyingi. “Nakuuliza hivi, pamoja na kutokuwepo kwa baraza la mawaziri umeshasikia Mtanzania amekufa kwa kukosa chakula. Acheni kuwatia hofu wananchi.
Rais atakapokuwa tayari atalitangaza kwa kuwa ndiye mwenye shughuli hiyo.’’  Hata hivyo, taarifa zilizolifiki Mwananchi jana zilieleza kwamba Rais Kikwete anatarajia kutangaza leo asubuhi baraza lake baada ya kazi ya ushauri wa kiufundi wa namna ya muundo wake, kukamilika jana.
Tetesi zilizolifikia gazeti hili pia zilieleza kwamba baraza hilo jipya limepunguzwa kutoka wizara 27 hadi kufikia 23. Baraza hilo pia linaelezewa kuwa na mawaziri kamili 23 wakati idadi ya manaibu inatarajia kupungua na kuwa kati ya 20 hadi 22.
Pia imeelezwa kuwa baraza hilo jipya, ambalo litakuwa la tatu kwa Rais Kikwete tangu alipoingia Ikulu mwaka 2005, litakuwa na manaibu waziri watano waliopandishwa kuwa mawaziri kamili. Vyanzo vyetu pia vimebainisha kuwa idadi ya mawaziri wanawake itaongezeka kulinganishwa na baraza lililopita na kwamba uteuzi umezingatia umri, uzoefu pamoja na uwiano wa mikoa.
Pamoja na kuwepo kwa sura mpya, idadi kubwa ya waliotajwa katika baraza hilo ni wanasiasa wakongwe ambao wengi wao walikuwamo katika baraza lililopita. Wabunge wanaotajwa kuingia kwenye baraza jipya ni Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), Samuel Sitta (Urambo Mashariki) ambaye alikuwa spika wa Bunge la Tisa, Dk Harrison Mwakyembe (Kyela) na Anne Kilango (Same Mashariki).

Wengine ni Januari Makamba (Bumbuli) ambaye alikuwa msaidizi wa Kikwete kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Salehe Pamba (Pangani), Steven Masele (Shinyanga Mjini), Gerson Lwenge (Njombe Magharibi) na Nyambari Nyangwine (Tarime).
Wengine ni Shamsi Vuai Nahodha (mbunge kuteuliwa) na alikuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Angela Mkwizu (Viti Maalum) na Amos Makala (Mvomelo) ambaye ni mweka hazina wa CCM, Said Bwanamdogo (Chalinze), Lazaro Nyarandu (Singinda Kaskazini) na Zakia Meghji (wa kuteuliwa na rais).
Akilihutubia Bunge Alhamisi iliyopita, Kikwete alidokeza kuunda serikali  itakayokuwa na watu waadilifu, makini na wachapakazi hodari. Pia alisema ataunda serikali ya watu wachache ambao itakuwa na mwelekeo wa kuwa karibu na wananchi na kushirikiana nao kikamilifu katika kuleta maendeleo na kupambana na umasikini.

0 comments: