Dk. Slaa atoa sharti

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeipa serikali sharti la kufanya mazungumzo ya kumaliza utata uliotokana na kinachodaiwa kuwa uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi.
Kimesema kiko tayari kukutana na serikali ilimradi ikubali kuunda tume huru ya kuchunguza uhalali wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuunda upya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuandika Katiba mpya.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, katika Ofisi za chama hicho, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alisema utayari wa CHADEMA kukutana utatokana na utayari wa serikali kukubali mapendekezo hayo, ili kujiridhisha na kuwapa haki Watanzania wanaolalamikia mfumo wa uchaguzi na katiba mbovu.

Alisema azma ya CHADEMA ni kushinikiza mabadiliko ya Katiba kabla ya 2015 ili kuepusha shari inayoweza kutokea siku za usoni kutokana na dhuluma inayolindwa na mfumo wa Katiba na sheria.

Alisema haikubaliki kimantiki kwamba matokeo ya ubunge yanaweza kuhojiwa lakini ya rais hayawezi kuhojiwa, hata kama kuna kasoro za wazi.

Alisema pia kuwa si sahihi kuacha Tume itangaze mshindi wa urais hata kama ameshinda kwa kura moja tu, kama ilivyo sasa. Anapendekeza mfumo uruhusu mshindi apatikane kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote.

Alisema pia ni vema Watanzania wapatiwe majibu kwa nini Tume ilitangaza kuwa waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 20, lakini waliojitokeza ni milioni nane (8); jambo ambalo linatia shaka kwamba huenda kulikuwa na hila katika mfumo mzima wa uchaguzi.

“Ninaamini kwamba kama umeshindwa kupigiwa kura na Watanzania wapatao asilimia 70, ujue wananchi hawakupendi, na nchi haiwezi kutawalika,” alisema Dk. Slaa.

Hata hivyo, alisema kutokana na kasoro hizo pamoja na nyingine zilizomo katika Katiba, kuna ulazima wa kuwapo kwa Katiba mpya ili chaguzi zitakazofuata zifanyike kwa uhuru na haki.

Hivi karibuni CHADEMA ilitoa tamko la kutoyatambua matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na NEC kwa madai kuwa taratibu nyingi zilivurugwa na Tume hiyo kwa lengo la kumbeba mgombea wa chama tawala, Rais Kikwete.

Alisema ingawa katika kipindi hicho cha kutangaza matokeo ya rais, CHADEMA iliipelekea NEC malalamiko ya kutoridhika na kuitaka isitishe na wao kuendelea kwa kukubali kasoro za jimbo moja la Geita ni udhaifu.

Msimamo wa tamko hilo ulionyeshwa kwa vitendo mwishoni mwa wiki iliyopita na wabunge wa chama hicho walipotoka kwenye ukumbi wa Bunge mara baada ya Rais Kikwete kuanza kuhutubia.

Wakati huo huo, moto umewaka ndani ya chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku baadhi ya wanachama wakiachia ngazi za uongozi na uanachama, na uongozi wa juu ukijipanga kuweka mikakati ya kikijenga chama kuelekea 2015.

Wakati juzi mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya, Sambwee Shitambala, akitangaza kuachia ngazi kupisha uchunguzi wa tuhuma kwamba ameuza chama, jana mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Taifa (Bawacha), Leticia Mosore, alijiondoa kwenye chama hicho baada ya kukosa ubunge wa Viti Maalumu, akajiunga na NCCR-Mageuzi.

Akijibu hatua za Shitambala na Mosore, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, jana alitoa kauli mbili, moja ikimzuia Shitambala kujiuzulu uongozi; na nyingine ikiainisha vigezi vilivyotumika kuwapata wabunge wa Viti Maalumu baada ya Bawacha, chini ya Mosore, kushindwa kuendesha uchaguzi huru na wa haki.

Dk. Slaa, alimtaka Shitambala kubaki katika nafasi yake, huku chama kikichunguza tuhumu dhidi yake za ‘kuuza ubunge’ wa Mbeya Vijijini, zikiendelea kufanyiwa kazi. Shitambala alituhumiwa na wanachama wenzake mkoani Mbeya kwamba alikosa ubunge kwa sababu aliuza nafasi hiyo kwa CCM. Juzi alitangaza kujiuzulu ili uchunguzi ufanyike dhidi yake.

“Hakuna haja ya wewe ndugu Shitambala kujiuzulu na kuruhusu makao makuu kufanya uchunguzi. Ofisi yangu itaendelea na uchunguzi wake kadiri, kwa wakati na, jinsi itakavyohitajika.

“…Kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA Ibara ya 6.3.4(a) sababu na msingi wa kujiuzulu kwako havijitoshelezi, hivyo unatakiwa kuendelea na nafasi yako kama unavyoelezwa na Katiba kisha kufafanuliwa na kanuni ya 7.71(i)-(iv),” ilieleza sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Dk. Slaa.

Kuhusu Mosore, aliyekuwa Diwani wa Viti Maalumu wa Tarime, Mara, alijiunga na CHADEMA miaka mitano iliyopita akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM), vongozi wenzake wa Bawacha mkoani Mara, walisema hawakushtushwa na Leticia kuhama chama hicho, kwa sababu walijua kwamba yeye alikuwa anasaka uongozi na maslahi binafsi, badala ya maslahi ya chama.

Mosore alitangaza azma yake ya kujivua uongozi na uanachama wa CHADEMA, mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi, Ilala, Dar es Salaam. Baadaye kidogo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alimkabidhi kadi na katiba yao.

Mosore aliwalaumu viongozi wa juu wa CHADEMA kwamba ndio waliomkosesha ubunge. Hata hivyo, uongozi wa CHADEMA ulisema Mosore alishindwa kuandaa uchaguzi wa kuwapata viti maalumu, hadi chama kikalazimika kuweka vigezo vipya.

Ingawa Mosore alidai kuwa kwa wadhifa wake wa mwenyekiti wa Bawacha alistahili kuwa Mbunge, viongozi wa CHADEMA na kwa mujibu wa vigezo vilivyotumika, hiyo haikuwa sifa pekee ya kumwezesha kuwa mbunge.

CHADEMA kilivunja uchaguzi wa Bawacha kikidai yalijitokeza mazingira ya rushwa na vurugu, hivyo kikaamua utafutwe utaratibu mpya wa kuwapata viongozi.

Awali, chama kiliamua kuweka kaulimbiu ya “asiyefanya kazi na asile” kwa maana kuwa wanawake wangepata ubunge huo baada ya kushiriki kikamilifu katika kampeni kwenye kata, majimbo na taifa.

Lakini wakati kampeni zinaendelea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilikitaka CHADEMA kuwasilisha majina ya wateule wake siku 30 kabla ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria; hivyo kikaunda utaratibu wa kitaalamu wa kuwapata kwa kumtumia Dk. Kitila, aliyeweka vigezo vilivyowapa alama kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho.

Dk. Willibrod Slaa, alisema Leticia hakubahatika kuwa miongoni mwa wanachama 25 wa kwanza walioomba Viti Maalumu, kwa sababu wenzake walimzidi katika vigezo sita (6) viliyowekwa, na mtaalamu elekezi; na kwamba haikuwa kazi ya viongozi wa juu kuteua majina ya wagombea.

Alisema kulingana na alama walizopewa wagombea, wa kwanza alipata 94 na wa mwisho mwiongoni mwa wanachama 105 waliopendekezwa, alipata alama 16. Wanawake wa CHADEMA walioomba nafasi za Viti Maalumu walikuwa 147, na nafasi zote kwa vyama vyote ni 105.

Idadai ya wabunge wa Viti Maalumu ilitegemea idadi ya wabunge wa majimbo, na kwa kuwa CHADEMA ilipata wabunge wa majimbo 24 kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) zilipatikana nafasi 25 za Viti Maalumu na alama za Mosore hazikutosha – labda kama wangepata wabunge wengi zaidi.

Dk. Slaa alisisitiza pia kuwa si viongozi wa chama waliohusika na kuteua majina ya wagombea, bali wagombea walichujwa kwa vigezo vilivyowekwa na mtaalamu elekezi aliyeombwa na chama kuwaandalia mchakato wa kuwapata wagombea, Dk. Kitila Mkumbo.

Vigezo vilivyotuma ni kiwango cha elimu, uzoefu wa uongozi ndani na nje ya siasa, mchango katika chama, umri katika chama, uzoefu wa uongozi wa siasa, uzoefu wa uongozi nje ya siasa, mchango wa hali na mali katika operesheni za chama na kampeni.

Ingawa Mosore, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC) ya CHADEMA taifa alisema kuwa kwa nafasi alizokuwa nazo alistahili kupata ubunge wa viti maalum lakini kwa madai yake alinyimwa nafasi hiyo kwa ubinafsi wa viongozi, wenzake walisema hivyo ni vigezo vya CCM, si CHADEMA.

Wakati hayo yakiendelea, CHADEMA inajipanga kuweka mpango mkakati wa kujiimarisha kutoka chini hadi taifa, na kukiimarisha chama kwa kazi kueleka 2015.

Miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujadiliwa katika vikao vitakavyofanyika siku chache zijazo, mahali patakapopangwa, ni jinsi ya kutumia nguvu iliyopatikana kujenga chama na kusahihisha kasoro zilizojitokeza mwaka huu.

Azima ya CHADEMA ni kuwasha moto wa mabadiliko makubwa ya Kikatiba na kisheria ambayo kimekuwa kinayalilia kwa miaka zaidi ya 18 iliyopita; na ambayo kimeanza kuyashinikiza kwa njia mbalimbali ikiwamo kumsusa Rais Jakaya Kikwete Bungeni, kwa madai kuwa amerejea madarakani kwa uchakachuaji wa kura.

0 comments: