
WAZIRI Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba amesema udini unaotajwa kuwapo nchini, hasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, umo miongoni mwa viongozi si wananchi wa kawaida.
Kauli hiyo ya Jaji Warioba ni sehemu ya maoni yake ya maadhimisho ya miaka 49 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, Desemba 9, mwaka 1961 yanayofanyika kesho Alhamisi.
Amesema licha ya viongozi waasisi kufanikiwa kujenga Taifa moja, dalili za sasa si njema na kwamba kasi ya viongozi kugawanyika hata katika vyama vyao vya siasa inaelekea kutishia umoja wa nchi.
Katika mahojiano maalumu na Raia Mwema yaliyochapishwa katika kurasa za tisa na 10 za toleo hili, Jaji Warioba anasema wananchi kawaida wamekuwa wakiendelea na shughuli zao bila kuulizana dini wala kabila zao.
“Wanafanya shughuli zao za kawaida iwe za biashara au uzalishaji. Ukikuta kundi la Wamachinga utawakuta vijana wa kutoka sehemu mbali mbali, dini mbali mbali na kabila mbali mbali wanafanya shughuli moja, hawajibagui hata kidogo.
“Inapofika wakati wa uchaguzi ndipo unasikia haya mambo ya ukabila, ukanda na udini. Haya yanaletwa na hawa ambao wanatafuta madaraka. Hawa wanaotafuta madaraka ndio wameleta matumizi ya fedha katika kutafuta uongozi,” alisema Jaji Warioba.
Katika hatua nyingine, Jaji Warioba ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, ameonyesha kukerwa na tabia mpya ya kutojiamini kama nchi kiasi cha kutegemea zaidi wafadhili.
“Kwa nini waasisi wetu walijiamini zaidi kuliko sasa hivi? Mimi nadhani wakati ule TANU inadai Uhuru tukiwa vijana ndiyo tumeingia kwenye siasa, hali ilikuwa ngumu sana.
“Watu wengi walikuwa wanasema huyu Nyerere anahangaika…hana uwezo wa kupambana na Mwingereza amuondoe. Kwamba bila msaada hauwezi kumuondoa Mwingireza lakini walijiamini na Uhuru ukapatikana.
“…sasa hivi hatujiamini tunazungumzia sana ufadhili, Serikali inazungumzia ufadhili, wananchi wanazungumzia wafadhili. Tumekuwa na imani kuwa hatuwezi kufanya chochote bila kuwa na wafadhili.
“ Nadhani tunachohitaji sasa ni kubadili akili na mtazamo wetu. Lazima tujiamini hata raia nao wanasema Serikali itufanyie hivi na hivi. Ni lazima tuanze kujiamini mtu mmoja mmoja mpaka jumuiya nzima.
“ Kama tunaendelea hivi na katika nchi tunasema kuna partners in development (wadau wa maendeleo) maana yake sisi hatuwezi kushughulikia maendeleo yetu bila hao wabia na ubia huo uko wapi zaidi?
“ Sina matatizo na mfadhili ambaye anataka kujua fedha alizotoa zimetumika vizuri, lakini nadhani wafadhili wengi wanatia masharti ambayo ndiyo yanaamua ni sera ya aina gani tuwe nayo na kuitekeleza.
“ Ni kama tumepoteza uwezo wetu wa kuamua sera zetu. Nadhani tuanze kuwa wakorofi katika eneo hili. Inawezekana, kwamba siku hizi mwananchi hahusishwi sana katika kuunda sera zetu, inakuwa ni viongozi na hawa wanaoitwa partners wanakubaliana kisha ndiyo inapelekwa kwa wananchi wakubali au wakatae na mara nyingi wanakubali. Inabidi sasa tuanze kuwa na kiburi kile tulichokuwa nacho.”
Katika kusisitiza anaongeza: “Naamini kama tukiamua kwamba hapana, mambo ya sera tutaamua wenyewe, siamini kama hawa wafadhili watatulazimisha tuwasilikize, lakini nadhani tumezoea hii ya wafadhili.
“Uhuru wetu sasa unaanza kupungua, kwa mawili yale tuliyoanzisha…umoja wa nchi na uhuru wa kuamua mambo ya nchi yetu tukaweka misingi, haya yameanza kuingiliwa.”
Alionyesha pia kutofurahia kuingia mwaka wa 49 wa Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika wakati vyombo vya dola Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zikiwa zinaingiliwa kisiasa.
0 comments:
Post a Comment