
RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, amevunja ukimya baada ya kusema ili kuzuia mifarakano ya kisiasa kwa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, zinahitaji kuwa na Katiba mpya, ikiwemo Tanzania.
Mkapa alisema hayo katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa jumuiya uliofanyika mjini Bujumbura nchini Burundi, mwezi uliopita.
Kwa mujibu wa taarifa ya Rais Mkapa, iliyosomwa kwa niaba yake na Balozi Liberata Mulamula, njia pekee ya kuondokana na migogoro ya kisiasa kila nchi inapaswa kuwa na Katiba mpya ambayo itaainisha mambo yote ya msingi.
Alisema kama nchi wanachama zikiwa na Katiba mpya mambo mengi yanaweza kufanikiwa, lakini yameshindikana kutokana na nchi hizo kuendelea kutumia Katiba zilizorithi kutoka kwa wakoloni.
Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kutokana na chaguzi nyingi toka kwa wanachama jinsi zinavyoendeshwa, huku shutuma na lawama nyingi zikielekezwa kwenye Katiba zilizopo.
Alisema Katiba zilizopo zimekuwa zikipendelea zaidi upande mmoja ambao unampa uhuru rais kuamua kila kitu.
Alisema uundwaji wa Katiba, lazima uendane na hali halisi, mahitaji ya kijiografia, kijamii na kisiasa.
“Tunakabiliwa na mtihani mkubwa wa kuunganisha umoja wetu wa kitaifa… kuna baadhi wamegusia juu ya matatizo yetu ya kisiasa na baadhi yetu tunafikiri kuwa siku ya kuadhimisha uhuru ni kilele cha kujenga umoja wetu wa kitaifa… uhuru wetu wa Katiba tulizonazo ni ushahidi wa dhuluma hii.
“…hatuna Katiba zingine zaidi ya zile ambazo tumezirithi kutoka kwa wakoloni, Katiba ambazo hazina umakini, tunahitaji mpya,” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ambayo Tanzania Daima imefanikiwa kupata nakala yake, Rais Mkapa alisema chaguzi nyingi zitakuwa huru na haki endapo kutakuwa na Katiba bora.
Akinukuu maneno ya mwandishi wa vitabu duniani (hakumtaja), ambaye pia ni mwanafalsafa aliyesema, ‘Chaguzi za Haki ni muhimu kwa Katiba bora.’
Alisema katika uundaji wa Katiba mpya, ni lazima kuwepo makubaliano maalum, kwa pande zote za kisiasa, kijamii na kijiografia, huku kanuni pamoja na mambo muhimu yakizingatiwa.
Alisema malumbano na migororo ndani ya nchi, yanasababishwa na muundo wa Katiba zinazoonekana kutokidhi haki na usawa.
“Katiba ndiyo moyo wa nchi, moyo wa mwanadamu unaofanya mwili mzima ufanye kazi… hivyo kwa kuangalia mbele tunahitaji kuundwa kwa Katiba na mihimili yote ya nchi, tunahitaji Katiba huru itakayotulinda katika hatari,” alisema Mkapa.
Akitoa mfano, Rais Mkapa alisema kumekuwa na sakata la uanzishaji wa Mahakama ya Kadhi katika nchi za Tanzania na Kenya, huku akisistiza kama lingekuwa ndani ya Katiba isingesababisha malumbano makubwa.
Kauli ya Rais Mkapa, imekuja wakati watu wa kada mbalimbali wakiwemo, wanasiasa, wasomi na wanaharakati wakiishinikiza serikali kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo, kwa madai kuwa haikidhi matakwa.
Mwanzoni mwa wiki hii, Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Celina Kombani, alisema hakuna haja ya kuwa na Katiba mpya, kitendo kilichoonekana kupingwa na watu wengi.
Waziri Kombani alisema Katiba iliyopo itaendelea kutumika kwani, serikali haina fedha za kufanya maandalizi ya kubadilisha Katiba hiyo.
Jaji Mkuu mstaafu Mark Bomani naye juzi alivunja ukimya na kusema kinachoisumbua serikali iliyoko madarakani ni woga ambao hauna msingi wowote.
Alisema Katiba iliyopo kwa kiasi kikubwa imepitwa na wakati, kwani wakati huu inakinzana katika baadhi ya vifungu, huku ikishindwa kutoa picha halisi ya demokrasia na utawala bora.
Naye Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanaharakati maarufu, Issa Shivji, amekuwa mstari wa mbele kupiga kelele mara kwa mara kutaka serikali ibadilishe Katiba iliyopo kwa manufaa ya taifa.
Mwaka 1998 Kamati ya White Paper iliyoundwa chini ya Jaji Robert Kisanga ilipendekeza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya, lakini ilipowasilisha ripoti yake ilikemewa kwa kile kilichodaiwa ilivuka mipaka kwa sababu ilikuwa kamati na si tume. Na hiyo ilikuwa awamu ya Rais Mkapa.
0 comments:
Post a Comment