Mbali na picha hiyo, simu ya mezani imekatwa waya na kichwa chake kubebwa; vitasa, zulia mafaili yenye nyaraka za maendeleo ya jimbo na mapazia vimeondolewa na watu wasiojulikana.
Kuibwa kwa samani hizo zilizogharimu fedha nyingi kutoka ofisi ya Bunge kulibainika jana baada ya mbunge mpya wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), kuingia rasmi kwa ajili ya kuanza kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, Wenje alilaani vikali kitendo hicho na kuvitaka vyombo vya dola kuchukua hatua za haraka kuchunguza na kuwatia mbaroni waliohusika.
“Ni jambo la kusikitisha kukuta samani za ofisi ya mbunge vimeibwa! Hali hii si ya kufumbiwa macho bali vyombo vya dola vifanye kazi yake kuchunguza wizi huu na hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika.
“…Ofisi ya mbunge ni mali ya umma kama ilivyo Ikulu (Ofisi ya Rais), fedha za walipakodi zinatumika kugharamia; sasa hivi vitu nani kaviiba?” alihoji Wenje kwa masikitiko.
Alisema, samani hizo zimeibwa katika kipindi cha siku mbili za hivi karibuni kwa kuwa aliwahi kufika kwenye ofisi hizo na kuzikuta baada ya kutoka bungeni.
Bila kutaja jina la mtu, Wenje alisema baada ya kubaini wizi huo, aliwasiliana na baadhi ya viongozi wa serikali ngazi ya wilaya na mkoa wa Mwanza, aliambiwa vifaa hivyo vilinunuliwa na mtu binafsi na havikuwa mali ya serikali.
“Niliwabana viongozi ngazi ya wilaya na mkoa wanieleze vimeenda wapi hivi vitu… niliambiwa eti vilinunuliwa na mtu binafsi na havikuwa vya serikali,” alisema mbunge huyo.
Alipotafutwa na Tanzania Daima kwa lengo la kutoa maoni yake juu ya madai hayo, aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha, hakupokea simu.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, kila mwezi mbunge hupokea kiasi cha sh 500,000 kwa ajili ya shughuli za jimbo ikiwemo ununuzi wa vifaa mbalimbali vya ofisi yake.
Akizungumzia fedha hizo, mmoja wa wabunge waliochaguliwa kwa mara nyingine, alisema kiasi hicho cha fedha hutumika kumlipa katibu wa mbunge na vifaa vya ofisi vinapohitajika.
“Hizo fedha tunapewa kila mwezi kwa ajili ya katibu wa mbunge, vifaa vya ofisi na vitu vingine ikiwemo posho ya dereva wa mbunge… lakini ofisi zetu nyingi ziko ndani ya jengo la mkuu wa wilaya kwa hiyo vitu kama meza na viti tunapewa na DC.
“…Picha ya rais huwa inatolewa bure, ni sehemu ya idadi ya vitu vinavyokuwemo kwa ajili ya kufungua ofisi. Ukikuta kuna simu au samani nyingine zinazoremba ofisi, wakati mwingine mbunge mwenyewe anaweka,” alisema mbunge huyo.
Katika hatua nyingine, Wenje alifanya ziara ya ghafla kwenye hospitali ya wilaya ili kujionea matatizo yanayoikumba hospitali hiyo, ikiwamo kukosekana kwa makabati ya kuhifadhi dawa.
Mbali na hali hiyo, pia mbunge huyo aliyekuwa anaongozwa na mganga kiongozi wa hospitali hiyo, Dk. Kajiru Muhando, alibaini kutokuwepo kwa kipimo cha X-Ray na kuona jinsi wagonjwa wanavyoketi chini kutokana na ukosefu wa mabenchi ya kukalia.
0 comments:
Post a Comment