Dk. Slaa, Mrema waponda uteuzi wa Kikwete

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa amekosoa uteuzi wa Baraza la Mawaziri kwa kusema kuna wizara zinazoundwa ili kufurahisha watu fulani.



Dk. Slaa amesema. Wizara hizo hazina kazi za msingi, hivyo ilitakiwa zipunguzwe ili kupunguza gharama za Serikali.

Amesema, kuundwa Baraza kubwa ni kuendeleza ufisadi ndani ya Serikali, kwa kuwa gharama kubwa itatumika kulihudumia kuliko kuwapelekea wananchi maendeleo.

Ametoa mfano wa Wizara ya Utawala Bora, akidai haina kazi yoyote ya msingi zaidi ya kuchapisha kijitabu kimoja kinachoonesha idadi ya kesi za rushwa nchini.

“Fikiria kuna wizara iliundwa akapewa Kingunge Ngombale-Mwiru, ikaitwa inajishughulisha na Mambo ya Siasa, lakini mpaka anaondoka madarakani, wizara hiyo haikuwahi kuonana na chama chochote cha siasa, sasa kuna wizara za aina hiyo nyingi kwa kufurahisha watu tu,” amedai mwanasiasa huyo.

Amesema, hata ukiangalia suala la kumpa uwaziri Samuel Sitta ni kwa ajili ya kumfurahisha, baada ya kutoteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kugombea uspika, hivyo ni lazima kuangalia maslahi ya wananchi na si kumfurahisha mtu mmoja.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema, amemuunga mkono Dk. Slaa kwa kusema kuwa Baraza lililoundwa bado ni kubwa na linazidisha matumizi ya kodi za wananchi bila sababu.

Amesema, licha ya kuwa kubwa, ikiwa mawaziri hao watawajibika na kufanya kazi kwa bidii, watamjengea heshima Rais kwa sababu ya kuwachagua na si kuchaguliwa wengi kisha hakuna kinachoonekana na Rais akimaliza muda kuondoka bila heshima.

Aliwataka mawaziri hao kuacha tabia ya kumwachia Rais kila kazi, kwani katika miaka ya hivi karibuni, kuna mawaziri walikuwa wakisubiri kazi za wizara zao kuingiliwa na Rais ndipo watekeleze.

Alisifia uteuzi wa vijana na wazee, akisema watu wanahitaji damu mpya itakayoleta mabadiliko katika Serikali.

0 comments: